

27 March 2025, 9:58 pm
Baadhi ya wanawake wilayani Hanang mkoani Manyara wamefundishwa namna ya kuandaa lishe bora ili kudhibiti tatizo la udumavu kwa watoto.
Na Mzidalfa Zaid
Katika kuhakikisha watoto wanakuwa na lishe bora, jamii wilayani Hanang mkoani Manyara imeshauriwa kuhifadhi vyema mazao,kwa kuhakikisha yanakaushwa vizuri na kutunzwa sehemu salama ili kuepuka vyakula hivyo kupata sumu kuvu.
Akiongea na wanawake wa Hanang pamona na wadau mbalimbali , mwanafunzi wa uzamivu NMAIST Naeliwa Mshanga amesema kwa utafiti walioufanya katika wilaya ya Hanang umebaini kuwa watoto wengi kuanzia umri wa miaka miwili wanakabiliwa na changamoto ya udumavu kutokana na kutopata lishe bora baada ya kufikisha miezi sita.
Kwa upande wake afisa kilimo wilaya ya Hanang Liberatus Msasa, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwani wananchi wengi walikuwa hawana uelewa wa kuhifadhi mazao yao sehemu salama, ambapo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima.
Nae mwakilishi wa mganga mkuu wa wilaya ya Hanang Ramla Kibwana Mang’ola amesema hali ya udumavu kwa watoto katika wilaya ya Hanang ipo kutokana na watoto hao kupata vyakula vya aina moja .
Baadhi ya wanawake wa wilaya ya Hanang ambao wamepata elimu hiyo, wamesema awali walikuwa hawajui namna ya kuandaa lishe bora pamoja na kuhifadhi salama chakula, hivyo elimu ambayo wameipata wataifikisha katika jamii inayowazunguka.