TFRA yatoa mafunzo ya usajili kwa maafisa ugani Babati
17 January 2025, 5:51 pm
Na Mzidalfa Zaid
Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) kanda ya kaskazini imetoa mafunzo ya usajili wa wakulima kwa maafisa ugani na kilimo wa halmashauri za wilaya ya babati na babati mji mkoani Manyara kupitia njia ya elektroniki.
Meneja wa TFRA kanda ya kaskakazini Gothard Liampawe, amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuongeza kasi ya usajili ili kusaidia maafisa ugani au kilimo kusajili wakulima wengi ndani ya muda mfupi.
Liampawe amesema kwa mkoa wa Manyara, wanatarajia kusajili wakulima lakitano na elfu tisa katika msimu huu wa kilimo na kwa sasa wakulima laki moja tu ndio wamesajiliwa ambapo amewataka wakulima kujisajili katika mfumo wa ruzuku ili wapate mbolea na mbegu kwa bei nafuu.
Amesema wametoa mafunzo hayo kwa washiriki 57 kupitia vishikwambi walivyogawiwa na serikali na matarajio ni kila afisa ugani asajili wakulima 5 kwa siku hivyo kwa mwezi kutakuwa na ongezeko la wakulima ambao wamesajiliwa.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo, wamesema elimu ambayo wameipata itawarahisishia kwenye kazi zao za usajili wa wakulima ambapo wamesema watatekekeza kwa wakati maelekezo waliyoyapata.