Serikali yawaonya wananchi watakaovuruga uchaguzi
27 September 2024, 7:35 pm
Wakati serikali ikiendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikli za mitaa, wananchi wilayani Babati mkoani Manyara wametakiwa kushiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu.
Na Mzidalfa Zaid
Wananchi wilayani Babati mkoani Manyara ambao wamekidhi vigezo vya kupiga kura wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la uandikishwaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi ambao utafanyikia Novemba 2024.
Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Shaaban Mpendu amesema Kwa mujibu wa sheria wakazi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na zaidi wanahimizwa kushiriki kwenye Uchaguzi huo kwa kuchukua fomu za kugombea au kupiga kura.
Kwa upande wake katibu tawala wilaya ya Babati Mkoani Manyara Halfan Matipula amewataka wananchi kushiriki uchaguzi huo Kwa amani na utulivu huku akiwataka viongozi wa vya siasa kuelemisha wanachama wao kufanya uchaguzi wa haki.
Aidha,mkuu wa polisi wilaya ya Babati Mkoani Manyara Ernesta Mwambinga, amesema Kila mwananchi anapaswa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo akiona kuna viashiria vya uvunjivu wa amani na kuwataka kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama unakuepo Kila wakati.