FM Manyara

Binti wa kazi za ndani anusurika kifo Manyara

June 15, 2024, 5:09 pm

Picha ya binti aliyefanyiwa ukatili na mwajiri wake

Wakati dunia ikielekea kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika Juni 16, 2024, binti wa miaka 15 mkoani Manyara amepigwa na mwajiri wake wakishirikiana na baba mwenye nyumba maeneo mbalimbali ya mwili  ikiwemo kichwani na miguuni kwa kutumia kisu, nondo na mbao.

Na Hawa Rashidi

Binti mwenye umri wa miaka 15  wilayani Babati mkoani Manyara amenusurika kifo baada  ya kupata kipigo kutoka kwa  mwajiri wake ambapo alikuwa anafanya kazi za ndani akimtuhumu kumuibia kiasi cha shillingi laki tatu ambazo zimechukuliwa na watoto wake.

Akizungumza na FM Manyara binti huyo ambaye amelazwa katika hospitali ya mji  wa  Babati Mrara  mkoani Manyara amesema  siku ya tukio mwajiri  wake alirudi kutoka kazini akiwa na pochi iliyokuwa na kiasi cha shillingi laki tatu na elfu hamsini na aliingia bafuni kuoga na alipotoka hakuikuta pochi yake, ndipo alipomtuhumu binti huyo kuwa kaiba pesa hizo na kuanza kumpiga kwa kutumia mbao, nondo  na visu akishirikiana na baba mwenye nyumba kumshambulia binti huyo.

Mtoto huyo amesema alimwambia mwajiri wake hajachukua pesa lakini aliendelea kumpiga maeneo ya kichwani pamoja na miguuni  na baada ya kipigo hicho alipata msaada kutoka kwa msamaria mwema ambaye ni jirani na nyumba anayoishi ambapo alimpeleka hospital ya Mrara kwa ajili ya matibabu kuanzia Juni 13, 2024.

Sauti ya mtoto aliyapigwa

Binti huyo amesema baada ya mwajiri wake kutafuta pochi aligundua watoto wake wenye umri wa miaka 8 na miaka 10 ndio walichukua pesa hizo kutoka katika pochi ya mama yao kwa kuziweka chini ya udongo karibu na nyumba yao.

Sauti ya mtoto aliyepigwa

FM Manyara ilimtafuta Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya  Babati mji Damian Matiku ili kuelezea hatua zilizochukuliwa baada yakufika Hospitalini hapo kutokana na taarifa alizopewa  lakini simu yake iliita bila kuwa na majibu.