Manyara kutoa chanjo saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti
21 April 2024, 12:01 am
Serikali imeanza kampeni ya chanjo ya mlango wa kizazi kwa mabinti kuanzia umri wa miaka 9 hadi 14 itakayotolewa katika shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo ili kuwaepusha na saratani ya mlango wa kizazi.
Na Hawa Rashid
Zaidi ya mabinti laki moja na nusu mkoani Manyara wenye umri kuanzia miaka 9 hadi 14 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ambayo inatolewa nchi nzima bila malipo ambapo wazazi na walezi wametakiwa kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya ili kupata njanjo hiyo.
Akizungumza na FM Manyara, Afisa elimu ya afya kwa umma mkoa wa Manyara Sweten Mwabulambo amesema chanjo hiyo ni muhimu kwa mabinti hao na zitatolewa katika shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo vyote vilivyopo mkoani hapa ambapo wataalam wa afya watafika katika maeneo hayo ili kutoa chanjo hiyo.
Amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeona umuhimu wa kuanzisha chanjo hiyo kwa lengo la kumkinga binti asipate saratani ya shingo ya kizazi ambayo imekuwa ni tatizo kwa akina mama nchini.
Aidha, amesema miongoni mwa mikoa itakayoadhimisha wiki ya chanjo kitaifa ni mkoa wa Manyara ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo utoaji wa chanjo za aina tofauti zitakazotolewa kwa mabinti na kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza.