Maafisa lishe, ustawi wa jamii watakiwa kutoa elimu ya malezi bora kwa watoto
23 February 2024, 5:53 am
Serikali mkoani Manyara imewataka maafisa lishe na maafisa ustawi jamii kutoa elimu kwa wazazi katika mikutano mbalimbali ya kijamii namna ya kumuandaa mtoto kwa kumlea katika malezi bora
Na Mzidalfa Zaid
Serikali mkoani Manyara imewataka maafisa lishe na maafisa ustawi jamii kutoa elimu kwa wazazi katika mikutano mbalimbali ya kijamii namna ya kumuandaa mtoto kwa kumlea katika malezi bora kuanzia anapokuwa tumboni ili kuandaa kizazi chenye maadili.
Wito huo umetolewa leo na katibu tawala mkoa wa Manyara Maryam Muhaji wakati akifungua kikao cha tathmini za utekelezaji wa shughuli za mpango wa program jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(MMMAM) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2023, kilichowakutanisha wataalam wa lishe, afya, elimu na maafisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri zote za mkoa wa Manyara.
Amesema vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vinavyotokea mkoani Manyara vinasababishwa na wazazi au walezi kushindwa kuwa karibu na watoto wao pamoja na kutowapa ulinzi wa kutosha na kuwataka wazazi kuhakikisha mtoto anapozaliwa anapata huduma muhimu za malezi ikiwemo kupata chanjo zote.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii mkoa wa Manyara Hadija Mhango , amesema hali ya ukatili katika mkoa wa Manyara bado iko juu, hivyo ili kukomesha vitendo hivyo jamii inapaswa kutoa taarifa wanaoobaini kuna vitendo vya ukatili vinafanyika.
Nae afisa mradi wa mtoto Kwanza kutoka shirika la COSITA Agustino Balhho , amesema kupitia mradi huo wamekuwa wakitoa elimu ya kupinga ukatili kwa watoto,namna ya kuandaa lishe bora kwa mtoto pamoja na malezi Bora ambayo mtoto anastahili.