FM Manyara

RC Sendiga atoa elimu ya bima ya afya kwa wote kaya kwa kaya

29 January 2026, 5:49 pm

picha ya Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Cuthbert Sendiga akitoa elimu kwa wananchi

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Cuthbert Sendiga akiwa na wataalamu wa Idara ya Afya ametembelea maeneo mbalimbali ya Mji wa Babati kwa ajili ya kutoa elimu na hamasa kwa wananchi Kujiunga na Bima ya Afya kwa wote.

Na Mzidalfa Zaid

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea na kutoa elimu ni pamoja na; baadhi ya Kaya kwenye Mtaa wa Majengo ya Zamani, Vijiwe vya mchezo wa Bao na kwenye Vijiwe vya waendesha Bodaboda, Bajaji na Guta.

Kupitia ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameelezea dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote wanapata uhakika wa kupata huduma za afya zilizo nafuu, sawa na zenye ubora.

sauti ya Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Cuthbert Sendiga

Mpango huo umeonekana kufurahiwa na wananchi ambao walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata majibu, hali iliyosababisha mwitikio chanya kwa kiwango kikubwa,na wakiunga mkono mpango huo wa Serikali.

Aidha, Wananchi wameiomba Serikali kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaenda sambamba na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya na hospitali, ili Bima hiyo iwe na tija kwa walengwa.

Wananchi hao pia wamemtaka Mkuu wa mkoa kuharakisha mchakato huo ili waweze kujiunga sawa na vigezo na masharti nafuu yaliyowekwa na Serikali kwa Kaya yenye watu 6 kuchangia kiasi cha Tsh 150,000 kwa mwaka mzima na kuwa na uhakika wa kupata huduma 372 za matibabu mbalimbali.