FM Manyara
FM Manyara
29 January 2026, 4:23 pm

Mkuu wa mkoa wa manyara, Queen Sendiga, amepinga takwimu ya asilimia 93 ya upatikanaji wa huduma za dawa mkoani Manyara , akisema si ya kweli kutokana na wingi wa malalamiko ya wananchi, huku akizielekeza halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zinafikisha elimu ya bima ya afya kwa wote katika kaya zote na makundi mbalimbali.
Na Mzidalfa Zaid
Ameyasema hayo , wakati wa kikao cha kuanza utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote ngazi ya mkoa wa Manyara, kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, na kuhudhuriwa na wadau wa afya, wakiwemo waganga wakuu wa wilaya, kamati zao pamoja na mganga mkuu wa mkoa.
Sendiga amesema kuwa huduma bora za afya zinakwenda sambamba na utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, ambapo wananchi hawapaswi kukumbana na malalamiko au kero yoyote.
Amewataka waganga wafawidhi, wakisimamiwa na mganga mkuu wa mkoa pamoja na waganga wakuu wa wilaya, kuhakikisha huduma zote muhimu, ikiwemo vipimo na dawa, yanapatikana katika hospitali na kwa wakati.