FM Manyara
FM Manyara
18 April 2025, 4:49 pm

Picha ya mkuu wa wilaya ya Babati
Mkuu wa wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda amewataka wataalamu wa halmashauri kukutana na viongozi wa wildlife management areas (WMA) pamoja na viongozi wa vijiji husika ili kuweka mpango wa pamoja wa kumaliza migogoro inayojitokeza mara kwa mara katika maeneo yaliyomegwa kiholela, hususan katika kijiji cha Vilima vitatu.
Na Mzidalfa Zaid
Kaganda ameyasema hayo katika kikao kilichoandaliwa na jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Burunge (JUHIBU) kwa viongozi wa vijiji vilivyopo ndani ya maeneo ya WMA (wildlife management areas), kwa lengo la kutoa uelewa wa pamoja kuhusu matumizi sahihi ya maeneo hayo na kuweka mikakati ya uendelevu kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi (GMP).
Amesema hatua iliyopo kwa sasa ni utekelezaji wa GMP, ambapo vijiji vimeshapatiwa elimu kuhusu matumizi ya maeneo yao Kupitia GMP,hivyo wananchi na viongozi wanapaswa kufahamu na kuheshimu alama maalum zitakazowasaidia watumiaji wa WMA kutambua maeneo na matumizi yake ili kusaidia uendelevu wa rasilimali zilizopo.
Kwa upande wake, mwanasheria wa halmashauri amesisitiza ufuataji wa sheria na taratibu zilizowekwa katika utekelezaji wa shughuli zote za ardhi na uhifadhi, na kuhimiza maridhiano pindi inapotokea migogoro ili kulinda amani na mshikamano katika jamii.
Katika kikao hicho, wajumbe walipata nafasi ya kufanya mijadala mbalimbali iliyoendeshwa mbele ya Mkuu wa Wilaya, kwa lengo la kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu majukumu yao, changamoto zilizopo na namna bora ya kushirikiana katika kusimamia maeneo ya WMA kwa manufaa ya wote.
