FM Manyara

Ruwasa Manyara yaadhimisha wiki ya maji kwa kutoa elimu

20 March 2025, 3:55 pm

Ruwasa Manyara yaadhimisha wiki ya maji kwa kutoa elimu.

Wakala wa usambazaji maji na usafi mazingira vijijini mkoa wa Manyara yawataka wananchi kutunza vyanzo vya maji.

Na Mzidalfa Zaid

Wakati wiki ya maji ikiendelea kuadhimishwa , wananchi Mkoani Manyara wametakiwa kutunza vyanzo vya maji kwa kutofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi karibu na vyanzo vya maji.

Wito huo umetolewa na meneja wa Ruwasa mkoa wa Manyara James Kionaumela wakati akiongea na fm Manyara, amewataka wanananchi kutofanya shughuli za kilimo, kukata miti au kuchunga mifugo karibu na vyanzo vya maji.

Amesema mkoa wa Manyara umeadhimisha wiki ya maji kwa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza uoto wa asili huku akisema upatikanaji wa maji vijijini kimkoa umefikia asilimia 78.09.

Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii Ruwasa mkoa wa Manyara Amina Mwanja, amesema kwa mkoa wa Manyara wana vyombo vya watumia maji ngazi ya jamii 49 ili kuhakikisha kila mwananchi wa kijijini  anapata maji safi na salama.

Wiki ya maji huadhimishwa kila mwaka ifikapo march 16 hadi 22, ambapo kwa mwaka huu kilele cha wiki ya maji kitaadhimishwa mkoani dare es salaam na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘kuhifadhi uoto wa asili kwa uhakika wa maji”