

4 March 2025, 6:22 pm
Na Mzidalfa Zaid
Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8 mwaka huu, wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara wametoa misaada kwa watoto njiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara na hospitali ya mji wa Babati (Mrara).
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo kwa niaba ya wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Babati, afisa maendeleo ya jamii na mratibu dawati mtambuka halmashauri ya mji wa Babati Ivetha Qamara, amesema wametoa msaada huo ili kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya miezi tisa.
Kwa upande wake katibu wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara pamoja na madaktari wa watoto kutoka hospitali ya Mrara wamewashukuru wanawake hao kwa kuonyesha upendo watoto hao ambao wanahitaji uangalizi.
Aidha, baadhi ya wazazi ambao wamepewa misaada hiyo wameomba taasisi zingine na makundi mbalimbali kuiga mfano huo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ambapo wamesema misaada hiyo itawasaidia katika kuendelee kuwalea watoto wao.
Maadhimisho ya siku ya wanawake ngazi ya mkoa yatafanyika machi 5, 2025, mwaka huu katika halmashauri ya wilaya ya Mbulu kauli mbiu ikisema wanawake na wasichana 2025, tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji.