Zaidi ya wananchi 350 Manyara wapatiwa huduma ya macho
10 October 2024, 5:11 pm
Mganga mfawidhi wa hospital ya halmashauri ya mji wa Babati(Mrara) Dr Gillian Francis Lupembe amesema Idadi ya wagonjwa waliokwenda kupata huduma ya matibabu ya macho imekuwa kubwa kutokana na watu wengi wanachangamoto ya uoni.
Na Marino Kawishe
Zaidi ya wananchi Mia tatu hamsini wamepatiwa huduma ya uchunguzi wa macho kwenye hospital ya halmashauri ya mji wa Babati Mrara iliyopo mkoani Manyara kwenye clinic ya madaktari bingwa wa macho inayoendelea kwa siku mbili.
Akizungumza na Fm Manyara Mganga mfawidhi wa hospital ya halmashauri ya mji mrara Dr Gillian Francis Lupembe amesema Idadi hiyo imekuwa kubwa kwasababu watu wengi wanachangamoto ya uoni na wataendelea kushirikiana na madaktari bingwa kila wakati kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake meneja program kutoka KCCO ambao ni waratibu wa kambi hiyo ya madaktari bingwa kutoka hospital ya KCMC mkoani Manyara na hospital ya rufaa mkoani Manyara Patricia Maaley amesema idadi hiyo inajumuisha watoto wa shule za msingi na sekondari ambao ni mia na hamsini na watu wazima zaidi ya mia mbili.
Nao baadhi ya wagonjwa waliojitokeza kupatiwa huduma za uchunguzi wa macho akiwemo mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya msingi Maisaka Nikolaus Marko amesema wataanza kufanyia kazi utoaji wa lishe bora kwa watoto shuleni ili kuwakinga na magonjwa ya macho ambayo yanaweza kuepukika.