Madereva bodaboda kuhamasisha ushiriki uchaguzi serikali za mitaa
27 September 2024, 7:11 pm
Waendesha pikipiki mkoani Manyara wamesema wako tayari kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ili kumchagua kiongozi bora.
Na Mzidalfa Zaid
Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara imefanya uhamasishaji kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwachagua viongozi bora.
Uhamasishaji huo umefanyika kwa njia ya kutembelea maeneo mbalimbali ya halmashauri ya mji wa Babati ambapo viongozi wa halmashauri hiyo wameambatana na kundi kubwa la maafisa usafirishaji wakiwa na pikipiki zao , ambapo afisa utumishi halmashauri ya mji wa Babati Gasto Silayo ambae amemuwakirisha mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Babati, amesema lengo la zoezi hilo ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa maafisa usafirishaji wa pikipiki mkoa wa Manyara Omari adam, amewataka waendesha pikipiki wote kufikisha elimu kwa wananchi kwenye maeneo wanakoenda kwakuwa ni mabalozi wakubwa ambao wanakutana na wananchi wengi.
Aidha, kwa upande wake afisa uchaguzi halimashauri ya mji wa Babati Bashan Kiyunyu amesema kutakuwepo na matukio mbalimbali likiwemo zoezi la uadikishaji ambalo linatarajia kuanza october 11 hadi 20 na kutafuatiwa zoezi la uteuezi wa wagombea, kampeni za uchaguzi pamoja na kufanyika uchaguzi.