Viongozi wa dini Manyara walia na maadili mabovu
20 May 2024, 9:18 pm
Ili kuendelea kuwa na maadili mazuri katika familia, wazazi wametakiwa kuwalinda watoto wao na kuwapa malezi bora kwa kushirikiana na jamii kwa pamoja ili kusaidia kuwa na kizazi bora katika jamii.
Na Hawa Rashid
Viongozi wa dini mkoani Manyara wameitaka jamii kusimamia vizuri malezi ya watoto wao na maadili mema kuanzia hatua za makuzi kwa kuwa hatua hiyo ni muhimu ambapo mtoto anapokuwa mdogo anakuwa mwepesi kuelewa anachofundishwa.
Akizungumza na FM Manyara Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mohamed Kadidi amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa kwa jamii kwa kufundisha masomo maalum ambayo yanapelekea ujenzi wa familia bora kwa kuwa dini ni mfumo wa maisha na wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao kwa kuwapa chakula, mavazi na mahitaji mengine.
Kwa upande wake Dkt. Padri Aidan Msafiri ambaye ni Mkurugenzi wa Vijana Jimbo Kuu la Moshi amesema kwa sasa familia nyingi zimekuwa na changamoto kubwa na zenye mzazi mmoja kwa kutengana baina ya familia na shule nyingi ni za kibiashara tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na malezi katika shule.
Aidha Padri Msafiri amesema kwa sasa jamii imekuwa na ubinafsi kwa kuwa kila mmoja anafikiria mambo yake na hakuna malezi ya pamoja na kusema suala la utandawazi limekuwa na changamoto kwa wazazi kuwapa simu watoto wao. Ameongeza kuwa uwajibikaji wa pamoja unahitajika katika malezi.