Radio Jamii Kilosa

Wananchi wahimizwa kukata kadi za bima ya afya – RC Morogoro

17 December 2020, 9:13 am

Wananchi Wilayani Kilosa na Mkoa wa Morogoro kiujumla wamehimizwa kukata kadi za bima ya afya kwa ajili ya familia zao kwani kadi hizo ni muhimu na zinasaidia kupata matibabu kwa urahisi hata nyakati ambazo mtu anakuwa hana fedha kwa ajili ya matibabu

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Loata Ole Sanare akizungumza na wananchi wa Kilosa

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati akikabidhi madawati 160 kwa shule za msingi nne,mashuka vipande 3278 na kadi za bima ya afya ICHF na NHIF vyote vikiwa vimefadhiliwa na shirika la World Vision ambalo linafanyua kazi katika Tarafa za Magole na Ulaya kupitia miradi mbalimbali katika sekta ya afya,lishe,maji,elimu na utetezi.

Licha ya kushukuru kwa ajili ya vifaa hivyo Sanare amesema kuwa Serikali inatambua misaada mbalimbali inayotolewa na World Vision lakini pia amelitaka shirika hilo kuendelea kufanya kazi na Halmashauri huku akiliomba kuongeza wigo wa kufanya kazi kwa mapana zaidi katika tarafa nyingine wilayani Kilosa na mkoa wa Morogoro.

Aidha amesema mkoa wa Morogoro umeweka mkakati wa kuwa na shule ya bweni hususani kwa shule za sekondari ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vishawishi vinavyopelekea kupata mimba wakiwa shuleni na kukatisha ndoto zao ambapo ametaka kuwepo kwa ushirikiano baina ya Serikali na wazazi ili kufanikisha jambo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Adam Mgoyi amesema shirika hilo limekuwa mdau namba moja katika kutoa misaada mbalimbali ili kupambana na umasikini ambapo wamekuwa wakitoa elimu katika shughuli mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo kutoa elimu ya kilimo cha kisasa na cha kibiashara lakini pia wamekuwa washiriki wazuri katika kukabiliana na majanga mbalimbali kama vile janga la Corona.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro kwa niaba ya shirika la World vision Meneja Mradi Elisei Chilala amesema shirika hilo limetoa madawati 160 yenye thamani ya shilingi 13,216,000,kadi za bima ya afya za ICHF kwa watoto 3,000 zenye thamani ya shilingi 15,000,000,kadi za NHIF kwa watoto 10 wenye mahitaji maalumu zenye thamani ya shilingi 504,000 na mashuka vipande 3278 kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi vikiwa na thamani ya shilingi 24,585,000.