Mufindi FM

Madiwani Mufindi DC wapitisha bajeti ya Bil 72.6

26 February 2026, 18:58

Pichani ni Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi wakiwa kwenye kikao cha kupitisha rasimu ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika Februari 25, 2026 katika ukumbi wa makao makuu ya halmashauri yaliyopo kijiji cha Itulavanu. Picha na Isaack Nyigo.

Maandalizi ya rasimu ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imezingatia miongozo mbalimbali ikiwemo Dira ya maendeleo ya taifa, Ilani ya CCM.

Na Marko Msafiri

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi limepitisha rasimu ya mpango na Bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2026/2027 yenye Jumla ya Shilingi Bil 72, 690, 102, 000 katika kikao chake cha Baraza kilichofanyika Februari 25, 2026 katika makao yake makuu yaliyopo katika kijiji cha Itulavanu.

Akiwasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Afisa Mipango na Uratibu Ndg. Elisey Ngoi, amesema kuwa, kati ya fedha hizo shilingi Bil 10.342 yatakuwa ni makusanyo ya ndani, shilingi Bil 6.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo fedha za nje na Bil 6.9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu.

Sauti Elisey Ngoi

Aidha Ndg Ngoi amesema bajeti hiyo imezingatia vipaumbele mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi, matengenezo ya miundombinu ya barabara hasa sehemu korofi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi ambayo haijakamilika, kuboresha miundombinu ya afya na kadhalika.

Hali Kadhalika, baraza hilo limepitisha rasimu ya mpango na bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya shilingi Bil 3, 485, 255,000 kwa ajili ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Mufindi.

Pia kwa upande wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), baraza hilo limepitisha rasimu ya mpango na bajeti ya shilingi Bil 2.1 kwa mwaka huo mpya wa fedha wa 2026/2027 ikiwa imepungua ikilinganishwa na bajeti wa mwaka 2025/2026 ambayo ilikuwa ni Bil 3.1.

Baada ya baraza la madiwani kupitisha bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Castory Masangula amesema rasimu ya bajeti hiyo inapaswa kuwekewa jitihada mahususi, kufuatia bajeti hiyo kutegemea sana mapato ya ndani ili kufikia malengo, huku akisisitiza zaidi kuhusu ukusanyaji wa mapato.

Sauti Mhe. Castory Masangula

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi Mhe. Castory Masangula katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Februari 25, 2026. Picha na Isaack Nyigo.

Naye Mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Mhe. David Kihenzile ambaye ni Naibu waziri wa Uchukuzi amekishauri kikao cha baraza hilo la madiwani kuunga mkono hoja ya uanzishwaji wa mnada katika eneo la Nyololo, lililopo wilayani Mufindi, kama sehemu ya kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Sauti Mhe. David Kihenzile

Kwa upande wao madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Makungu Mhe. Felix Lwimbo amesema bajeti waliyoipitisha inakwenda kuwakomboa wananchi na changamoto mbalimbali huku Diwani wa Kata ya Mbalamaziwa, Mhe. Aida Kaduma ameongezea kuwa bajeti ya sasa imegusa kila kata hasa katika aneo la miundombinu ya barabara.

Sauti Madiwani