Mufindi FM

Waziri Mchengerwa awaasa wanahabari, bima ya afya kwa wote

3 February 2026, 12:40

Pichani ni Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa Vyombo vya habari na Waandishi wa Habari kuhusu Bima ya afya kwa wote kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee mkoani Dar es salaam. Picha na Christogon Ngoloki.

Na Christogon Ngoloki

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amevitaka vyombo vya habari kutumia kalamu zao kama nyenzo ya kuelimisha jamii kwa lengo la kuwa na uelewa sahihi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kunufaika kikamilifu na huduma za afya.

Waziri Mchengerwa amezungumza hayo, katika kikao kazi na Wahariri pamoja na Wakurugenzi wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika Jijini Dar es salaam, kwa lengo la kujadili na kutoa ufafanuzi kuhusu mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Sauti Mchengerwa 01.

Mhe Mchengerwa Ameongeza kwa kusema kuwa afya ni ngome na ulinzi wa Taifa, hivyo ni wajibu wa wanahabari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya afya, hususan mpango wa bima ya afya kwa wote.

Sauti Mchengerwa 02.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema mpango wa bima ya afya kwa wote ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyotoa katika siku zake 100 za uongozi wa Awamu ya Sita.

Pichani ni Wahariri na Waandishi wa Vyombo vya habari ambao ni washiriki wa kikao kazi hicho cha Waziri wa afya Mhe. Mchengerwa kuhusu Bima ya afya kwa wote. Picha na Christogon Ngoloki.

Ikumbukwe kuwa tarehe 23 Januari mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitangaza rasmi kifurushi cha mafao ya huduma muhimu za afya, ambapo kila kaya itachangia shilingi laki moja na nusu kwa mwaka kwa ajili ya wanachama sita wa familia moja.

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote na kuhakikisha jamii inapata huduma za afya kwa gharama nafuu na kwa wakati.