FM Manyara
FM Manyara
24 October 2025, 8:47 pm

Kaya (28) za maeneo ya Msasani Maisaka A na Maisaka Kati Wilayani Babati, mkoa wa Manyara zimelipwa fidia ya bilioni 2.9 baada ya maeneo yao kuchukuliwa na serikali kwa matumizi ya huduma za kijamii.
Na Mzidalfa Zaid
Taarifa ya malipo ya fidia hiyo zimetolewa na Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga kupitia kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo amewashukuru na kuwapongeza wananchi hao kwa kuridhia kuyaachia maeneo hayo ya vyanzo vya maji kwa manufaa ya jamii nzima ya wakazi wa Wilaya ya Babati ambao hutegemea chanzo hicho.
Amewataka wananchi hao kuridhika na kiwango kilichotolewa na serikali Baada ya kufanyika kwa tathmini ya mwisho mwaka 2024 huku akiwaahidi kuwapatia viwanja vya bei nafuu vilivyopimwa na kuwasihi wananchi hao kutumia fedha hizo za fidia kujenga makazi mapya na kujiendeleza kiuchumi.
Aidha, baadhi ya wananchi hao Kupitia kikao hicho wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiaga kwa kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu malipo ya fidia ya maeneo yao .
Wamesema kuwa wamekaa muda mrefu tangu mwaka 2008 pasipo kujua hatma yao ambapo wameushukuru uongozi wa Serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kukata kiu yao ya muda mrefu.
Aidha, Sendiga ametoa muda wa miezi sita kwa wananchi hao kuondoka kwa hiari kwenye maeneo hayo ili Mamlaka ya Maji Babati (BAWASA) waanze kutekeleza mradi mkubwa wa usambazaji wa maji katika Mji wa Babati.