FM Manyara

Mwenge wa uhuru kutembelea miradi ya zaidi ya shilingi billion 10 Babati

11 July 2025, 9:52 pm

Picha ya mkuu wa wilaya Babati Emmanuel Kaganda

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, amesema Mwenge wa Uhuru 2025 utatembelea na kukagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 10 katika Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Babati Babati Mji na Babati DC.

Na Mzidalfa Zaid

Akizungumza  katika kipindi Cha Mseto wa kwo kinachorushwa kupitia kituo cha redio cha FM Manyara,  Kaganda amesema miradi hiyo ni ya sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, miundombinu ya maji, barabara, na uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.

Sauti ya Mkuu wa wilaya Babati Emmanuel Kaganda

Amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaoanza Wilayani humo Julai 14 kupitia Babati DC na kuendelea Julai 15 kwa Babati Mji. Mwenge huo pia utazindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua utekelezaji wa miradi hiyo.

Kaganda amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru ni chombo muhimu cha kuhamasisha maendeleo, uzalendo na mshikamano wa kitaifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki na kujifunza.

 Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru 2025 ni:  *“Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”*