

14 March 2025, 6:39 pm
Mkuu wa wilaya ya Babati mkoani Manyara Emmanuela Kaganda amefurahishwa na uwekezaji uliofanyika katika kijiji cha Sangaiwe ambao umetokana na jitihada za wananchi wa kijiji hicho.
Na Mzidalfa Zaid
Mkuu wa wilaya ya Babati mkoani Manyara Emmanuela Kaganda amekagua miradi mbalimbali ambayo imejengwa katika kijiji cha Sangaiwe kupitia mapato ya serikali ya kijiji hicho yatokanayo na uhifadhi.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo Kaganda amesema kijiji hicho kimekuwa cha kwanza nchi nzima kwa utunzaji wa uhifadhi ambapo amesema kwa mwaka 2021 hadi 2025 zaidi ya shilingi bilioni 2.4 zimekusnywa na fedha hizo kutumika katika miradi ikiwemo ujenzi wa shule,ofisi ya kijiji pamoja na zahanati.
Amesema miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto ya migogoro kati ya wananchi na wanyama ambapo changamoto hiyo ilitatuliwa baada ya wananchi kukaa kwa pamoja na kujadili namna ya kutunza uhifadhi ambapo kwa sasa kijiji hicho kimeendelea kutokana na uwekezaji unaoendelea.
Kaganda àmetoa wito kwa vijiji vingine vyenye changamoto ya uharibifu wa uhifadhi kufika katika kijiji cha Sangaiwe kujifunza ili kupata ujuzi namna ya kutumia uhifadhi kuleta maendeleo katika maeneo yao na kuepuka migogoro kati ya wanyama na binadamu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Sangaiwe Marian Mwanso amesema kupitia mapato hayo kijiji kinachangia fedha za kumsomesha mwanafunzi anaefaulu kuingia kidato cha tano au chuo pamoja na kuwanunulia vyakula wanafunzi.
Aidha,mganga mfawidhi wa zahanati ya kijiji hicho Latifa Maida amesema mapato hayo ya uhifadhi yamesaidia kujenga majengo mapya ya zahanati na amezungumzia changamoto ya barabara inayofika zahanati hapo hali inayopelekea wanachi kukosa huduma kwa haraka.
Akisoma risala mbele ya mkuu wa wilaya ya babati, kaim mtedaji wa wa kijiji hicho joseph hosea, amesema kijiji hicho kina jumla ya wawekezaji 5 ambao wanasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi katika kijij hicho.