Wananchi tunzeni wanyama pori
22 October 2024, 6:31 pm
Serikali yasema imeweka mazingira yakuvutia wageni kupitia filamu ya royal tour ambapo watalii wameongezeka hasa mkoani Manyara nakuleta fedha nyingi za kigeni ambazo zinanufaisha vijiji hivyo.
Na Marino Kawishe
Wananchi waishio karibu na hifadhi za taifa za Manyara na Tarangire wametakiwa kuendelea kulinda mazingira na wanyama pori wanaowazunguka ili kuendelea kunufaika na mapato yatokanayo na uhifadhi kwenye vijiji vyao.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameyasema hayo katika kilele cha fainal ya chem chem ligi soka iliyofanyika katika uwanja wa mdori uliopo Vilima vitatu kata ya Mwada, ambapo amesema kila mwaka vijiji vipatavyo kumi hupatiwa mgao wa fedha zaidi ya shillingi milion mia moja kwa kila kijiji kutoka kwa jumuiya ya uhifadhi ya Burunge.
Amesema serikali kupitia rais Dr Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira yakuvutia wageni na kupitia filamu ya royal tour watalii wameongezeka hasa mkoani Manyara nakuleta fedha nyingi za kigeni ambazo zinanufaisha vijiji hivyo.
Kwa upande wake afisa mahususiano kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Chem chem Association Charles Sylvester amesema kwa mwaka huu wa 2024 fainal hizo zimeongozwa na kauli mbiu inayosema tunza mazingira okoa twiga ikimaanisha jamii inapaswa kushirikiana na wawekezaji hao katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya uhifadhi.
Aidha,huu ni msimu wa kumi tangu kuanzishwa kwa mashindano yanayodhaminiwa na taasisi ya chem chem association na kwa mwaka huu yakijumuisha zaidi ya timu 35 kutoka vijiji kumi ambavyo ni Mdori, Mwada, Ngoley, Vilima vitatu, Kakoi, Minjingu, Manyara,Olasiti na Sangaiwe. na bingwa wa mchezo wa soka kwa wanaume ikiwa ni timu ya majengo kutoka kata ya mwada iliyoshinda magoli mawili kwa moja dhidi ya boda boda fc ya magara.