FM Manyara

Jela miaka 22 kwa kukutwa na nyara za serikali Babati

10 September 2024, 5:22 pm

Hakimu wa mahakama ya wilaya ya Babati Victor Kimario amewahukumu Richard Lutema (49) na Moses Cosmas (28) kwenda jela kwa kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya shillingi millioni 600,ambapo walikaatwa may 21 mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni ya kasablanka iliyopo mjini Babati

Na George Augustino

Mahakama ya wilaya ya Babati mkoani Manyara imewahukumu Richard Lutema (49) na Moses Cosmas (28) kwenda jela miaka 22 kila mmoja  kwa kosa la kukutwa na vipande nane vya meno ya tembo ambavyo ni nyara za serikali.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya mahakama hiyo hakimu Victor Kimario amesema watu hao walikutwa  na nyara hizo za serikali zenye thamani ya zaidi ya shillingi milioni 600 na walikamatwa Mei 21 mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni ya Casablanca iliyopo mjini Babati mkoani Manyara wakiwa wamehifadhi katika begi la rangi ya kijivu.

Hakimu Kimario amesema watu hao walikamatwa na jeshi la polisi baada ya jeshi hilo  kupata taarifa kwa mtu aliyekuwa akiwatilia shaka watu hao ndipo upekuzi ukafanyika katika chumba walichofikia.

Kwa upande wake wakili wa serikali Bernadeta Mosha ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao kwa kuwa vitendo vya  ujangili vimekithiri na vinaisababishia serikali hasara kwa kupoteza mapato kupitia utalii wa wanyama pori.

Aidha, Hakimu Kimario amesema mahakama hiyo  imezingatia ukweli kuwa kosa hilo ni la kwanza kwa watuhumiwa na wana wategemezi  kwenye familia lakini wametumia nguvu zao kwenda kufanya ujangili na  mahakama imewahukumu kifungo cha miaka 22 kwenda jela kila mmoja..