Jela miaka 24 kwa kukutwa na nyara za serikali
21 May 2024, 11:38 pm
Hakimu wa wilaya ya Babati Mkoani Manyara Victor kimario awahukumu kwenda jela miaka 24 kila mmoja Fred Meibuko (28) mkazi wa mvugue mkoani Tanga na Issa mafita (30) mkazi wa wilayani Babati kwa kosa la kukutwa na jino moja la tembo.
Na George Agustino
Mahakama ya wilaya ya Babati mkoani Manyara imewakukumu kwenda jela miaka 24 Fred Meibuko (28) mkazi wa mvugue mkoani Tanga na Issa mafita (30) mkazi wa gedamara kata ya gallapo wilayani Babati kwa kosa la kukutwa na jino moja la tembo ambalo ni nyara ya serikali kinyume cha sheria.
Akisoma shauri hilo la jinai mbele ya mahakama hiyo hakimu wa wilaya ya Babati Victor Kimario amesema watuhumiwa hao walikutwa na kosa hilo la kukutwa na nyara hiyo ya serikali yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 49 tarehe 4 novemba mwaka jana 2023 majira ya saa 6 mchana katika eneo la gallapo wakiwa wanasafirisha kuelekea Babati kwa kutumia usafiri wa pikipiki.
kwa upande wake wakili wa serikali Leonce Bizimana ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ambayo itakuwa ni fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo kwakua mnyama tembo anahusika katika utalii na analiingizia taifa fedha za kigeni kutoka kwa watalii.
Naye wakili wa utetezi Abdalla Kilobwa ameiomba mahakama kuwapunguzia kifungo washtakiwa hao ambao bado ni vijana na wananguvu za kufanya kazi kwa kuwa ndio kosa lao la kwanza kushtakiwa .
Aidha akitoa hukumu hiyo hakimu Kimario amesema kwa kuzingatia utetezi wa upande wa washtakiwa hao na upande wa utetezi wa serikali mahakama hiyo imejiridhisha pasi na shaka na imewakukumu kwenda jela miaka 24 kila mmoja na kuamuru jino hilo la tembo kukabidhiwa kwa mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori kwaajili ya kutunza ushahidi na kuliweka katika kumbukumbu za serikali