Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
24 November 2026, 7:57 am

Wizi wa shata katika shule nne Hasanga wazua hofu kuhusu usalama wa miundombinu ya elimu.
Na Pili Mwang’osi
HASANGA
WIZI wa shata za madirisha katika shule nne za Kata ya Hasanga, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, umeibua changamoto ya ulinzi wa miundombinu ya elimu na kuhatarisha juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Diwani wa Kata ya Hasanga,Mh.Malick Nzowa, akizungumza na wakazi wa kata hiyo kupitia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Shule ya Msingi Isangu na Sekondari ya Hasanga, Mh.Nzowa amesema vitendo hivyo vimeanza kujitokeza katika Shule ya Msingi Ipogolo na baadaye kuathiri shule nyingine.
Amesema wameanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi katika maeneo ya shule, huku akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini na kuwachukulia hatua waliohusika.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo Janet Mwashiuya na Geofrey Nzunda, wamesema vitendo hivyo vinakatisha tamaa na kurudisha nyuma juhudi za kuboresha mazingira ya elimu, wakisisitiza umuhimu wa jamii kulinda mali za umma.
Naye kiongozi wa dini, Yohana Filimon na Mwenyekiti wa Mila wa Hasanga, Dickson Njalo, wameeleza msimamo wao kuhusu vitendo hivyo.