Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
2 February 2026, 6:57 pm

Hafla ya uzinduzi na kukabidhi gari ya SORECU.
Na Devi Moses
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Makame, amezindua na kukabidhi gari la Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (SORECU), lililonunuliwa kwa fedha za chama hicho, katika hafla iliyofanyika leo tarehe 30 Januari 2026 kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nselewa, wilayani Mbozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Makame amepongeza uamuzi wa SORECU kununua gari hilo, akieleza kuwa hatua hiyo ni kielelezo na dhamira ya dhati ya kuimarisha shughuli za ushirika mkoani humo.
Kadhalika, Mhe. Makame amekumbusha umuhimu wa utekelezaji wa majukumu kwa uadilifu na uwajibikaji, akisisitiza kuwa uzembe au vitendo visivyo vya uaminifu vinaweza kuwa kikwazo cha maendeleo ya vyama vya ushirika na wanachama wake
Kwa upande wake, mjumbe wa SORECU ambaye pia ni Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Fredy Katoto, amesema chama hicho kilikuwa kinakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri, hali iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa baadhi ya shughuli.
Naye Meneja wa Shughuli za SORECU, Mon Mwampamba, amesema uwepo wa gari hilo utaongeza uwezo wa chama kuwafikia wanachama kwa wakati, jambo litakalosaidia kusikiliza na kutatua changamoto zao.