

April 23, 2025, 12:53 pm
Ubovu wa barabara wakwamisha wananchi kutofanya shughuli za maendeleo
Na Kennedy Sichone
HASANGA
Wananchi wa kitongoji cha Isangu kata ya Hasanga wilayani Mbozi mkoani Songwe wamelalamikia ubovu wa barabara ya kutoka Isangu kwenda kitongoji cha Iyela. Wakizungumza na Vwawa FM Radio, wananchi hao wamesema barabara hiyo imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa shughuli zao za kila siku, hasa upande wa usafiri wa abiria na mizigo.
Wananchi wamesema hali mbaya ya barabara hiyo inasababisha vyombo vya usafiri kama pikipiki na magari kuharibika mara kwa mara, hivyo kuongeza gharama za matengenezo kwa wamiliki wa vyombo hivyo. Aidha, wameeleza kuwa wakati wa mvua, barabara hiyo huwa haipitiki kabisa, jambo linalosababisha wananchi kushindwa kufikia huduma muhimu kama masoko, vituo vya afya na shule.
Akifafanua kuhusu kero hiyo, diwani wa kata ya Hasanga, Mheshimiwa Malick Nzowa, amesema tayari wamepokea fedha kutoka mfuko wa jimbo la Vwawa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo. Diwani amesema hatua za awali za maandalizi ya ukarabati huo zimeanza na wanatarajia kazi hiyo itaanza mara moja baada ya taratibu kukamilika.