Radio Jamii Kilosa

Mbunge wa Jimbo la Mikumi aongeza nguvu ujenzi wa Madarasa.

2 February 2021, 1:12 pm

Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo Kulia akikabidhi saruji kwa viongozi wa Shule za sekondari Kidodi na Lyahila.

Mbunge wa jimbo la Mikumi Mh. Dennis Londo amekabidhi mifuko 200 ya saruji katika shule ze sekondari Iwemba, Lyahira, Kidodi na Ruhembe ambapo kila shule imekabidhiwa mifuko 50 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono agizo la Waziri Mkuu la kuhakikisha kila shule inapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kidato  cha kwanza na kuwa na madarasa ya kutosha kwa ajili ya watoto hao waweze kusoma vizuri

Mbunge Jimbo la Mikumi Denis Londo Kulia akikabidhi saruji uongozi wa Shule ya Sekondari Iwemba.

Mh. Londo amekabidhi mifuko hiyo ya saruji Februari mosi mwaka huu katika shule hizo ambapo amesema ugawaji huo wa mifuko hiyo ni muendelezo wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Mikumi ambao hadi sasa umeshatoa mifuko 400 ya saruji ikiwa ni katika kuunga mkono jitihada za ujenzi wa vyumba vya madarasa ambazo unaoendelea katika shule mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo wapili kushoto akikabidhi saruji kwa viongozi wa Shule ya Sekondari Ruhembe.

Aidha amesema kuwa kwa upande wa shule ya sekondari Ruhembe mifuko 50 hiyo itatumika kuongeza nguvu katika ujenzi wa jengo la utawala kwani kwa sasa walimu wanatumia vyumba vya madarasa kama ofisi hivyo kufanikisha ujenzi  wa jengo la utawala kutafanikisha walimu kuwa na ofisi zao na hivyo kupelekea madarasa yanayotumika kama ofisi kuanza kutumika na wanafunzi kwa ajili ya masomo

Kwa upande wa diwani wa kata ya Kidodi Mh.  Abdulatif Kaid na diwani wa kata ya Ruaha  Mh. Alex Gwila  wamemshkuru mbunge wa Mikumi kwa namna ambavyo ameunga mkono kazi ya ujenzi inayoendelea katika kata zao na kwamba saruji hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kazi hiyo ambapo wanategemea baada ya ujenzi huo wanafunzi watakaa madarasani kwa nafasi bila kubanana kutokana na uwepo wa madarasa ya kutosha.

                                                                            Kaka Mkuu shule ya Sekondari Iwemba Salum Athumani

Naye Kaka Mkuu wa shule ya sekondari Iwemba Salum Athumani kwa niaba ya wanafunzi wa shule zote zilizopata mifuko ya saruji amemshukuru mbunge wa jimbo la Mikumi kwa namna ambavyo ameonyesha kuwajali kwa kuhakikisha shule zinakuwa na madarasa ya kutosha ambapo amesema anaamini kupitia uwepo wa madarasa hayo utawasaidia kukaa madarasani kwa nafasi na kujisomea kwa uhuru nyakati zote.