Radio Jamii Kilosa

Mkandarasi lukolo constrctor atakiwa kumaliza Mradi kwa wakati Kilosa -Kusaya.

16 January 2021, 4:49 pm

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akikagua Mradi wa skimu ya umwagiliaji Kata ya Kilangali Wilayani Kilosa.

Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya ametoa muda hadi ifikapo mwisho wa mwezi huu mkandarasi Lukolo Construction Ltd awe amekamilisha ujenzi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Kilangali ili itumike na Wakala wa Mbegu wa Taifa ( ASA) kuzalisha mbegu kwa mujibu wa mkataba.

Kusaya ametoa onyo hilo Januari 14 mwaka huu wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo unaotekelezwa chini ya mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa zao la mpunga ( ERPP) chini ya wizara ya Kilimo  ambapo amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi 11 ambapo miradi 10 ipo tayari isipokuwa wa Kilangali ambao kwa sasa umefikia asilimia 75 hivyo mkandarasi aongeze kasi ili ifikapo mwisho wa mwezi awe amekamilisha na kuukabidhi.

Kusaya amesema Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na Benki ya Dunia inatekeleza mradi wa Kuongeza tija kwenye zao la mpunga katika Wilaya za Mvomero,Kilosa na Ifakara ambapo skimu 5, maghala 5 na maabara moja ya kilimo zimejengwa na zitakabidhiwa kwa wakulima mwisho wa mwezi huu.

Aidha amesema mradi wa skimu ya Kilangali una ukubwa wa hekta 400 na unagharimu shilingi Bilioni 5 ambapo kupitia mradi huo na miradi mingine iliyo chini ya wizara hiyo inalenga kuwafanya wakulima walime kisasa  na waongeze tija na kukuza kipato .

Naye Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Morogoro Dkt.Rosalia Rwegasila amesema mradi wa ERPP umewezesha tija kuongezeka kwani uzalishaji Mpunga umeongezeka toka tani 400,000 mwaka 2016 hadi tani 800,000 mwaka 2020