Radio Fadhila
Radio Fadhila
1 July 2025, 8:11 AM

“Victor Francis alikuwa ni muumini wa muda mrefu wa kanisa hilo na alikuwa akihudumiwa kwa maombi na marehemu Mchungaji kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kutokana na matatizo ya kiafya“
Na Neema Nandonde
Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linamshikilia mkazi wa kijiji cha Lupaso kitongoji cha kadudu Wilaya ya Masasi mkoani humo Victor Francis (39), kwa tuhuma za mauaji ya mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblise of God (TAG) lililopo kijijini hapo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara SACP Issa Suleiman, amesema tukio hilo limetokea Juni 27, 2025 majira ya saa 12 jioni katika mtaa wa misheni kwenye kijiji hicho cha Lupaso.
Amemtaja marehemu huyo kuwa ni Thomas Rajab (58), ambapo siku ya tukio mtuhumiwa akiwa na baadhi ya ndugu zake alikwenda katika kanisa hilo, kwa ajili ya kupata huduma ya kiroho kutokana na changamoto ya kifafa ambayo inasadikika kuwa anayo matuhumiwa huyo, na baada ya kufanyiwa maombi kwa muda mrefu mtuhumiwa alionesha kuchoka.
Ameongeza kuwa, ndugu wa mtuhumiwa kwa kushirikiana na marehemu waliamua kumrejesha nyumbani kwa ajili ya kuendelea na maombi, walipokaribia nyumbani kwa mtuhumiwa, mtuhumiwa aliruka kwenye pikipiki na kukimbia kuingia ndani ya nyumba yake na kutoka na panga.
Aidha baada ya kutoka na panga, alianza kumkimbiza marehemu kisha kumkata na panga sehemu mbalimbali za mwili wake, na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake apo hapo.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na mara baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.