Mufindi FM

Madiwani Mufindi DC wahimiza ukusanyaji mapato, baada ya kubaini kushuka

13 February 2026, 13:44

Pichani ni Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi wakiwa katika kikao wakijadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika makao makuuu ya Halmashauri hiyo yaliyopo kijiji cha Itulavanu. Picha na Isaack Nyigo.

Naomba kitengo hiki cha mapato tusikifanyie mzaha maana ndiyo injini ya halmashauri”

Na Marko Msafiri

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Limebaini kushuka Kwa hali ya Ukusanyaji wa mapato ikiwa hadi sasa limekusanya asilimia 41.5 ya lengo, tofauti na wastani wa asilimia 50 uliokuwa unafikiwa katika kipindi kama hiki hapo awali.

Baraza hilo limeketi Februari 11, 2026 katika makao makuu yaliyopo katika kijiji cha Itulavanu, kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Castory Masangula amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kukisimamia kwa ukaribu kitengo cha mapato, akisema ndiyo kitengo mama kinachobeba utekelezaji wa shughuli nyingi za kimaendeleo katika halmashauri hiyo.

Sauti Mwenyekiti wa Halmashauri

Awali Diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Kasanga Mhe. Asunta Mtende amehoji ni lini halmashauri itatenga bajeti kwa viongozi hasa watendaji wa kata na vijiji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa misitu.

Kufuatia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Mashaka Mfaume ameiagiza Idara ya Maliasili na misitu kutenga bajeti kwa ajili ya uwezeshaji wa mafunzo kwa viongozi waishio katika maeneo yanayozunguka mashamba ya misitu kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi namna ya kulinda chanzo hicho cha mapato cha misitu.

Sauti DED Mufindi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Ndg. Mashaka Mfaume akiwa katika Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lililokuwa linajadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Picha Isaack Nyigo.

Naye Afisa Maliasili na Misitu wa wilaya hiyo, Ndg. Gilbert Ngailo ameeleza mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Halmashauri katika kudhibiti janga la moto katika misitu ikiwemo kufanya mikutano na mikoa jirani hasa wilaya ya Kilombero iliyozungukwa na shamba hilo la halmashauri, kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti majanga ya moto, akisema kwa mwaka uliopita ekari 150 kati ya 450 zimeteketea kwa moto.

Sauti Afisa Maliasili na Misitu.

Mhe. Grace Mgina, ambaye ni Diwani viti maalumu tarafa ya Sadani, amesema wao kama madiwani wameonelea haja ya kuanzisha kilimo cha miti kama chanzo cha mapato katika ukanda mwingine hasa wa joto ikiwemo katika tarafa hiyo, huku Diwani wa kata ya Kibengu Cley Msungu amesema amependekeza sheria kali kwa wale wanaotorosha au kuchoma moto mashamba ya misitu hasa ikizingatiwa halmashauri inapoteza mapato mengi kupitia moto.

Sauti Madiwani.