Mufindi FM

Jamii yatakiwa kuripoti ukatili bila kuogopa

15 July 2025, 19:02

Kulia ni Inspekta Wilfred Willa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto makao makuu ya polisi Dodoma akiwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi ambaye ni Mkuu wa dawati hilo mkoa wa Iringa ASP. Elizabeth Swai (kushoto) wakiwa Mufindi FM redio katika mahojiano maalum kuhusu masuala ya ukatili. Picha na Christogon Ngoloki.

Zamani matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto yalikuwepo, lakini yalikuwa hayaripotiwi kwa uwazi au kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa. Hali hii ilisababishwa na utamaduni wa kumaliza kindugu, uoga au aibu, kutokuwa na mifumo rafiki ya kuripoti na uelewa mdogo wa sheria.

Na marko Msafiri.

Jamii imesisitizwa kuripoti matukio ya ukatili kwa wakati, kutoa ushirikiano wa kutosha mahakamani na kuacha tabia ya kumalizana kindugu kwani jambo hilo linaficha matukio hayo katika jamii na kuendelea kushamiri kwa matukio hayo pasipo kupata suluhisho juu ya masuala hayo.

Hayo yamejiri wakati wa Mahojiano maalumu hapa Mufindi FM Radio na Inspekta. Wilfred Willa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma, ambapo amesema dawati hilo linafaya kazi kwa usiri mkubwa sana, huku akiihakikishia jamii kwamba hakuna chombo kingine zaidi ya mahakama inayotoa maamuzi ya matukio hayo.

Katika kuepusha matendo ya ukatili katika ndoa, Inspekta. Willa amewatahadharisha wana ndoa kuacha kupekua simu ya mwenza wake, akifananisha kitendo hicho kama nyoka alieingia pangoni.

Sauti Inspekta. Wilfred Willa.

Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. Elizabethi Swai ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Iringa amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili katika dawati ni ucheleweshaji wa kuripoti matukio ya ukatili, jambo linaloathiri Ushahidi, na kuitaka jamii kutoa taarifa mapema (saa 72), kuficha matukio hayo kwa kuogopa kuvunja mahusiano hasa pale mwenza mmoja anapotuhumiwa kufanya ukatili.

Sauti ASP. Elizabeth Swai.

Nae Polisi jamii wa wilaya ya Mufindi SP. Deogratias Shee ameongeza kuwa elimu inayotolewa kupitia njia mbalimbali kama redio imeongeza hamasa katika jamii ya kuripoti matukio ya ukatili ukilinganisha nah apo awali, huku akiisihi jamii kujishughulisha na kazi halali.

Sauti SP. Deogratias Shee