Mufindi FM
Mufindi FM
11 June 2025, 00:23

Wadau mbalimbali wakiwa picha ya pamoja wakiwemo watoa huduma, vyama vya ushirika, wafanya biashara, wasindikizaji wa mazao na maofisa wa serikali mara baada ya kuhitimisha mafunzo ya kikao biashara. Picha na Marko Msafiri.
Awali, wakulima wengi walikumbana na changamoto mbalimbali kuhusu masoko ya mazao, zikiwemo upungufu wa miundombinu, ukosefu wa taarifa za soko, kutegemea Madalali na ubora wa mazao.
Na Marko Msafiri
Kikao muhimu cha biashara kuhusu masoko ya mazao kimefanyika katika Hotel ya Midlands iliyopo Makambako mkoani Njombe kikiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka katika sekta ya Kilimo, biashara na huduma za kifedha wakiwemo watoa huduma, vyama vya ushirika, wasindikaji wa mazao, wafanyabiashara na wawakilishi kutoka serikalini.
Lengo kuu la kikao hicho ni kujadili kwa kina hali ya masoko ya mazao, fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau mbalimbnali kwenye sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Kikao hicho kimefanyika chini ya uratibu wa Taasisi ya Nafaka Kilimo kupitia mradi wa Kilimo Masoko unaosimamiwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili kuwawezesha wakulima kuinua kutoka daraja moja kwenda lingine.
Akizungumza Mratibu wa mradi huo Bw. Mosses Logani amesema lengo la kikao hicho ni kuwaunganisha wadau ili kuwezesha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wakulima na wanunuzi wakubwa wa mazao, na hivyo kujengwa uelewa wa pamoja kuhusu mahitaji ya soko.
Sauti Mratibu wa mradi
Kwa upande wake Afisa ubora kutoka Wakala wa Taifa ya Uhifadhi wa Chakula (NFRA) kwa niaba ya Meneja wa kanda ya Makambako mkoani Njombe Vicent Alfred Ndelwa amebainisha vigezo vinavyotumika katika ununuzi wa mahindi kwa wakulima.
Sauti Afisa ubora NFRA
Bw. Ndelwa amesema kwa mwaka huu, taasisi hiyo imejipanga kununua mahindi tani laki moja.