TGNP Manyara yamsaidia mzee aliyetelekezewa watoto
2 October 2024, 9:01 pm
Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP Mkoani Manyara umemsaidia mzee Tlaho Meho kumjengea nyumba kwakua mazingira anayoishi ni hatarishi kwake na watoto wadogo alioachiwa na mke wake aliyemtoroka.
Na Marino Kaweshe
Kituo cha Taarifa na Maarifa kinachofanya kazi zake kwenye kata ya Mamire wilayani Babati mkoani Manyara kimesema licha ya changamoto za kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wananchi kitaendelea kuzisaidia jamii za watu masikini na wasiojiweza.
Akizungumza na FM Manyara, Mratibu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP mkoani Manyara Clara Malley amesema miongoni mwa kazi wanazofanya ni kumjengea nyumba ya kuishi mwananchi mmoja ambaye makazi yake ni duni na huku akitelekezewa watoto wawili na mke wake ambaye amekimbia familia hiyo zaidi ya miezi mitatu sasa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Manyara WP Leokadia akizungumza na wanakikundi hicho cha taarifa na maarifa kutoka kata ya Mamire amesesitiza wananchi kuripoti matukio ya ukatili ambayo yanafanywa kwenye maeneo wanayotoka.
Kituo cha taarifa na maarifa cha mamire kipo katika hatua za awali kukamilisha ujenzi wa nyumba yenye chumba na sebule kwa mkazi wa kitongoji cha Gubuli katika kijiji cha Endagile kwenye kata ya mamire ambaye makazi yake ni duni na hayana hadhi ya kuishi binadamu.