World Vision wazindua mradi wa maji Gidabagara
24 March 2024, 4:29 pm
Wananchi wa kijiji cha Gidabagara waishukuru World Vision kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama
Na Christina Christian
Wananchi wa kijiji cha Gidabagara wilayani Babati mkoani Manyara wamelishukuru shirika la kimataifa la kikristo World Vision kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama.
Wakizungumza na fm manyara radio katika wiki ya huduma ya maji wananchi hao wamesema kuwa upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama kijijijini hapo umekuwa ni furaha kwao kwani walikuwa wakitumia maji ya mabwawa na visima visivyofunikwa ambayo hayakuwa salama hali iliyopelekea kupata magonjwa ya kuhara pamoja na wanafunzi kuchelewa masomo darasani .
Akizindua mradi huo mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga kwa niaba ya serikali amelishukuru shirika la World Vision na kusema kuwa jambo walilofanya ni la kuigwa na wadau wengine kwani mradi huo utafanya kazi kubwa kuwahudumia wananchi hao.
Mradi wa maji uliopo kijiji cha Gidabagara kata ya Boay wilayani Babati mkoani Manyara umegharimu jumla ya Tsh 291,669,700 na wanufaika ni wakazi 1509. Kupitia mradi huu shule ya msingi Gidabagara yenye wanafunzi 610 wasichana 279 na wavulana 331 imewezeshwa kupata mabomba ya maji safi na salama ili kulinda afya za watoto wawapo shuleni.