TIRA yawafikia wafugaji Manyara
28 October 2024, 6:25 pm
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA)kanda ya kati imewashauri Wafugaji mkoani Manyara kukata bima ili kujikinga na majanga yanapotokea.
Na Mzidalfa Zaid
Wafugaji mkoani Manyara wameshauriwa kukata bima ili kujikinga na majanga yanapotokea ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa ,mafuriko, magonjwa au sababu nyinginezo ambazo zinaweza kumsababishia hasara mfugaji.
Hayo yameelezwa leo na Afisa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA)kanda ya kati Gladys Steven wakati akiongea na FM Manyara amesema wafugaji wanapokuwa na Bima inawasadia kurudi katika hali yao ya kawaida wanapopata majanga.
Amesema TIRA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wakiwemo wafugaji juu ya umuhimu wa kuwa na bima kupitia vyombo vya habari, maonesho, semina na mikutano.
Kwa upande wao wafugaji ambao wametembelea banda la TIRA kwenye maonesho ya Manyara Tanzanite Trade Feir, wamesema awali walikuwa hawajui umuhimu wa wa kuwa na Bima hivyo elimu waliyopata imewapa ari ya kuamua kukata bima itakayowasaidia katika shughuli yao ya kifugaji.
Wamesema elimu hiyo waliyoipata wataipeleka kwa wafugaji wengine ambao hawana uelewa huku wakiiomba serikali kuendelea kutoa elimu mara kwa mara ili wapate miongozo namna ya kujiunga .
Nae afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka Mamlaka ya usimamizi wa Bima Anna Massao, amewataka wananchi kutembelea banda la TIRA ili wajifunze mambo mbalimbali ikiwemo kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka.
Amesema katika banda hilo wapo maafisa mbalimbali kutoka Mamlaka ya usimamizi wa Bima(TIRA) ambao wanatoa elimu inayohusu bima lakini zaidi wanaelimisha fursa zilizopo katika Soko Kama kuwa wakala au washauri wa bima.