Radio Jamii Kilosa

Meneja TRA Kilosa atoa siri ukusanyaji kodi .

20 April 2021, 10:40 am

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Kilosa Musa Harun akiwa katika mahojiano Radio Jamii Kilosa .

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kutoka kwa wafanyabiashara waliolipa kodi kwa wakati kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambako kumechangia kuongeza mapato katika Wilaya na kuiwezesha serikali kutimiza malengo ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Meneja wa TRA Kilosa Musa Haruni

Hayo yamesemwa April 20 ,2021 na Meneja wa TRA Wilaya ya Kilosa Musa Haruni alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Mambo mseto Kinachorushwa na Redio Jamii Kilosa kuhusu elimu kwa mlipa kodi.

Haruni amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha kuazjia mwezi julai 2019 hadi Machi 2020 TRA Kilosa iliweka malengo ya kukusanya kodi kiasi cha shilingi bilioni 2.9 ambapo walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 3.04 na kuvuka lengo na kwa kipindi hicho hicho Mwaka 2020/2021 walikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilion tatu Milioni miatano ishilini na moja laki sita tisini na moja elfu mia nane thelathini na moja nukta sifuli tisa (3,521,691,831.09) ambapo walikusanya shilingi Bilioni tatu Milioni mia sita themanini na nane laki sita sabini na sita elfu mia nne hamsini na nane nukta tisa sifuli (3,688,676,458.90) sawa na asilimia 104 na kumefanya kuwa na ongezeko la mapato Kiasi cha shilingi Milioni 639 .

Amesema kuwa Siri kubwa iliyopelekea kukusanya kuvuka lengo kwa miaka miwili mfululizo ni Kutoa elimu ya mlipa kodi Mara kwa Mara kupitia Redio , Luninga ,Kufanya matangazo ya mtaa kwa mtaa (PA) ,kupita mlango kwa mlango kwa wafanya biashara kwa ajili ya kutoa elimu hiyo na kumesaidia kujenga uelewa wa pamoja kuhusu ulipaji wa kodi .

Ameendelea kutoa Rai kwa walipa kodi kulipa kodi Stahiki kwa wakati na wale ambao hawajafika kukadiriwa mwaka huu na Wale waliofika lakini hawajalipa wafike walipe ili kuepuka adhabu huku akiwakumbusha wananchi wote kudai risiti wanaponunua bidhaa ama kupata huduma na wafanyabiashara kutoa risiti wanapouza.

Sambamba na hayo Haruni amewapongeza Wafanyabiashara wote ,Jumuiya ya Wafanya biashara Kilosa Ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa , Mkuu wa Wilaya ya Kilosa pamoja na taasisi za kifedha kwa ushirikiano waliotoa kuwezesha TRA na Serikali kwa ujumla kutimiza malengo yake.