Redio Fadhila wapigwa msasa uandishi unaozingatia maadili
9 January 2025, 11:25 PM
Waandishi wa habari wametakiwa kuandika habari kwa kuzingatia maadili ya uandishi ili kuepuka kuingia kwenye matatizo wakati wa uchaguzi mkuu.
Na Lilian Martin
Mhariri wa radio tadio Hilali Ruhundwa ametembelea kituo cha Radio Fadhila leo Januari 09, 2025 na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika kituo hicho.
Katika mafunzo hayo Ruhundwa amewakumbusha waandishi wa habari juu wa kuandika habari zinazozingatia maadili ya uandishi zaidi katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ameongeza kwa kusema kuwa mwandishi wa habari asipofuata maadili ya uandishi wa habari ni rahisi kuwa chanzo cha uchochezi na kuingia kwenye matatizo.
Sambamba na hayo mhariri wa Radio Tadio amewahimiza waandishi kulitumia jukwaa la kuchapisha habari (radio tadio portal) kusambaza taarifa na vipindi vinavyoendelea katika radio husika ili kutangaza kituo na kuongeza wafuatiliaji wa vipindi katika radio husika.
Huu ni mwendelezo wa mafunzo ya ndani yaliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari (VIKES) toka Finland chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo na kuratibiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Vyombo vya Habari vya Jamii Tanzania (TADIO) ambapo licha ya kuwajengea uwezo redio wanachama namna ya kuchapisha habari mtandaoni, wanafundishwa pia namna ya kuandika habari wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu hapa nchini.