Radio Fadhila
Radio Fadhila
07/03/2026, 10:13

Wanawake wanayo haki ya umiliki wa mali yoyote kama mwanaume ila jamii nyingi katika maswala ya imani huwakandamiza wanawake hasa katika umiliki wa Ardhi
Samia Ardhi Clinic kupiga kambi siku saba Masasi Mji kuelekea Siku ya Wanawake
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi, Halmashauri ya Mji wa Masasi imeanza kutoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wanawake kupitia mpango wa Samia Ardhi Clinic, utakaopiga kambi kwa muda wa siku saba. Maadhimisho ya mwaka huu yalianza tarehe 2 Machi na yatafikia kilele chake tarehe 8 Machi.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Booster cha Fadhila Redio, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Mwasobe Machota, amesema kuwa katika wiki hiyo ya maadhimisho wataendelea kutoa elimu pamoja na msaada wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi kwa wanawake ili kuwawezesha kutambua na kutumia haki zao.
Ameeleza kuwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na elimu ya ardhi, uhamisho wa umiliki wa ardhi, taratibu za kuendeleza ardhi, utoaji wa hati kwa waliokamilisha taratibu, pamoja na kuhuisha hati zilizokwisha muda wake. Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanawake wote ndani ya Halmashauri ya Mji wa Masasi kupata uelewa wa haki yao ya kumiliki ardhi kama inavyotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 24.