Radio Fadhila

Juhudi za polisi kupunguza ukatili na vitendo vya uhalifu Masasi

05/03/2026, 14:51

Jeshi la Police wakitoa Elimu

Katika kuendelea kutimiza majukumu yao ya kazi kwa jamii leshi la Polisi Masasi inaendelea kuwakumbusha wanafunzi kuhusu kujiepusha na matukio ya kikatili

Na Lilian Martin

Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Kitengo cha Dawati la Jinsia wilayani Masasi, Ziada Mponela, ametembelea chuo cha Sayansi shirikishi Masasi Cohas kilichopo Masasi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na maadili kwa wanafunzi

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho, Mponela amesisitiza umuhimu wa kutambua aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia na kiuchumi, huku akiwataka vijana kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo hivyo katika jamii.

Aidha, amewataka wanafunzi hao kuzingatia sheria za nchi na kanuni za chuo kwa kuacha tabia ya wizi na vitendo vingine vinavyokiuka maadili, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuharibu mustakabali wao kitaaluma na kimaisha.

“Nyinyi ni wataalamu wa afya wa kesho. Jamii inawaamini. Jilindeni na mjilinde dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na uhalifu,” amesisitiza Mponela.

Wanafunzi wa Masasi cohas

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa jamii, hususan kwa vijana waliopo mashuleni na vyuoni, ili kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia na uhalifu katika Wilaya ya Masasi.