Radio Fadhila
Radio Fadhila
14 November 2025, 10:13 AM

“Mtuhumiwa huyu ambaye ni Katibu wa UVCCM kata ya Namalenga licha ya kumchoma moto mtoto wake wa kambo, lakini pia amemuadhibu vibaya mtoto mwingine ambaye alishirikiana nae wakati wa kuuza korosho”
Na Neema Nandonde
Salumu Hussein Maona mkazi wa kitongoji cha Temeke Mkangaula ambaye pia ni Katibu wa Vijana CCM kata ya Namalenga wilayani Masasi Mkoani Mtwara, amemchoma moto maeneo ya mikononi mtoto wake wa kambo Abdul Zahoro Paulo (11) mwanafunzi wa darasa la nne, baada ya kuiba korosho.
Akizungumza na redio Fadhila, Mwenyekiti wa kitongoji hicho Ismail Shaibu, amesema tukio hilo limetokea novemba 12, 2025 ambapo wazazi wa mtoto huyo waliondoka nyumbani na kumuacha mtoto huyo akiwa na watoto wenzake.
Baada ya baba kurejea, akagundua walipohifadhi korosho zimepungua, na alipofuatilia akabaini kuwa Abdul amechukua takribani kilo 3 na kwenda kuziuza kwa mnunuzi asiye rasmi kwa shillingi 4500.
Kufuatia hilo, Mtuhumiwa akafunga mikono ya mtoto huyo kwa kamba, na kufungua koki ya pikipiki yake kisha akamwagia petroli mikono hiyo ndipo alipompeleka ndani na kumchoma moto.
Kwa upande wa majirani na mashuhuda wa tukio hilo, wameeleza kuwa baba huyo ni kawaida kumfanyia matukio ya ukatili mtoto huyo, lakini mengi yamefichwa na mama yake na hili limethibitika kwakuwa ni kubwa zaidi.
Naye baba aliyefanya tukio hilo la kikatili, amekiri kutenda kosa hilo huku akijutia kuwa haikuwa adhabu nzuri kwa mtoto.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kitongoji cha Temeke Mkangaula, ameeleza kuwa taratibu nyingine za kisheria zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa baba huyo anaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.