Radio Fadhila
Radio Fadhila
22 September 2025, 7:50 PM

“Kama wana Masasi jumanne ya septemba 23, 2025 tuna kila sababu ya kwenda kumsikiliza mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, maana kuna mengi mazuri ameyatenda kwetu“
Na Neema Nandonde
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kimesema kimejipanga ipasavyo kwaajili ya ziara ya mgombea urais kupitia chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan siku ya septemba 23, 2025.
Katibu mwenezi CCM wilaya ya Masasi Twahili Said Mayola, ameyasema hayo septemba 22, 2025, alipokuwa anazungumzia ujio wa Dkt Samia kwenye kipindi cha Stendi Kuu kinachorushwa na redio Fadhila.
Aidha amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano mkubwa wa hadhara utakaoongozwa na Dkt Samia utakaofanyika kwenye uwanja wa Boma, ili wasikilize sera na mipango chanya ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo.

Sambamba na hayo Mayola amesisitiza kuwa, kutokana na kazi kubwa ya kuleta maendeleo nchini ikiwemo wilayani Masasi, iliyofanywa na serikali inayoongozwa na Dkt Samia, wakazi wa Masasi wana kila sababu ya kufurahia maendeleo hayo na kuunga mkono jitihada zilizofanywa na serikali hiyo kwa kumchagua tena Dkt Samia.
Mgombea urais kupitia chama Cha Mapinduzi Dkt Samia Suluhu Hassan ataanza rasmi ziara mkoani Mtwara siku ya septemba 23, 2025 hadi septemba 26, 2025 ambapo atafanya mikutano ya kampeni kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo Uwanja wa Boma wilayani Masasi.
