Radio Fadhila
Radio Fadhila
19 September 2025, 12:43 PM

Wakati mwingine wananchi hususani wanaoishi vijijini wanaishi kwa mazoea, kama mtu amezaliwa na kukulia kwenye nyumba isiyo na shimo la taka na yeye analazimisha aishi hivyo siku zote
Na Neema Nandonde
Kuelekea maadhimisho ya siku ya usafi duniani ambayo hufanyika kila ifikapo septemba 20, wananchi wa halmashauri ya wilaya Masasi mkoani Mtwara wametakiwa kuacha kupuuzia maelekezo ya usafi wa mazingira yanayotolewa na wataalam, ili kuondoa athari zitokanazo na mazingira machafu.
Hayo yameelezwa septemba 19, 2025 na Afisa Afya Mazingira Halmashauri ya Wilaya Masasi, Said Ame alipokuwa anazungumzia siku ya usafi duniani kwenye kipindi cha Fadhila Mseto kinachorushwa na redio Fadhila.
Kwa upande wake Afisa Afya Mazingira Halmashauri ya wilaya Masasi, Glory Masawe amezungumzia kaulimbiu ya siku ya usafi duniani kwa mwaka 2025 ambayo inasema “Tunza mazingira kwa kuzipa taka thamani” ambapo amefafanua kuwa si kila taka inatupwa moja kwa moja, bali zipo taka ambazo zinaweza kutumika tena baada ya kuziongezea thamani kwa kuzirejeleza au kubadilishia matumizi.
Sambamba na hilo amewataka baadhi ya wafanyabiashara kuacha tabia ya kutii amri ya kufunga maeneo ya biashara kwa muda kwenye siku maalumu za usafi, akiwasisitiza kushiriki kufanya usafi na si kubaki nyumbani na kusubiri muda wa kufungua maeneo hayo.

Halmashauri ya wilaya Masasi, inatarajia kuadhimisha siku ya usafi duniani katika kata ya Ndanda ambapo baadhi ya watumishi wa serikali, wananchi na taasisi zisizo za kiserikali watakutana kwa lengo la kufanya usafi wa mazingira kwa pamoja, huku wananchi wengine wakisisitizwa kufanya usafi kwenye maeneo yanayowazunguka.