Radio Fadhila
Radio Fadhila
5 August 2025, 3:30 PM

“Jamii iache kuishi kwa mazoea kwenye suala la malezi hususani unyonyeshaji wa maziwa ya mama ili kuwaandaa watoto wenye ukuaji bora kimwili na kiakili”
Na Neema Nandonde
Kufuatia maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani, jamii wilayani Masasi mkoani Mtwara, imeaswa kuzingatia unyonyeshaji sahihi wa maziwa ya mama pekee ili mtoto asipatiwe kinywaji au chakula chochote kabla ya kutimiza miezi 6.
Hayo yameelezwa Agosti 5, 2025 na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Masasi Omari Mushi, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila.
Amesema kuwa mtoto mwenye umri wa chini ya miezi 6, anapopewa chakula au kinywaji tofauti na maziwa ya mama, inasababisha michubuko kwenye mfumo wa chakula, jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa mtoto.
Sambamba na hayo, Mushi amefafanua kuwa kunyonyesha hakuharibu umbo la titi la mama, bali mama akinyonyesha kwa usahihi inamsaidia kuepuka saratani ya matiti na msongo wa mawazo.

Maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji ilianza rasmi Agosti 1, 2025 na kilele chake kitakuwa Agosti 7, 2025 huku kaulimbiu ikisema kuwa “Thamini Unyonyeshaji weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto”