Radio Fadhila
Radio Fadhila
26 June 2025, 11:19 AM

“Mnaweza kusafisha ufuta vizuri na mkaufunga kwenye vifungashio, lakini watu wasio waaminifu wakaenda mbele wakabadilisha vifungashio wakaweka uchafu, MAMCU tutalidhibiti hilo kwa kuzalisha vifungashio vyetu vitakavyohifadhi mazao moja kwa moja”
Na Neema Nandonde
Chama kikuu cha Ushirika MAMCU kinachohudumia wakulima wa wilaya ya Masasi, Nanyumbu na Mtwara mkoani Mtwara, kimedhamiria kuanzisha miradi mbalimbali itakayosimamiwa na chama hicho, ili kuondoa kero zinazowakabili wakulima wanaohudumiwa na chama hicho.
Hayo yameelezwa juni 26, 2025 na Mwenyekiti wa Chama hicho, Alhaji Azam Mfaume, alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila, ambapo amesema miradi hiyo ni ujenzi wa maghala mawili ya kukusanyia mazao wilayani Mtwara, kiwanda cha kutengeneza vifungashio na kusafishia ufuta wilayani Masasi, kituo cha kisasa cha malipo wilayani Nanyumbu na ununuzi wa malori kwaajili ya kusafirishia mazao ya wakulima.

Akizungumzia kushuka kwa bei ya ufuta kwa msimu unaoendelea ukilinganisha na msimu uliopita, Alhaji Mfaume ameeleza kuwa kama ilivyo biashara za kawaida, kuna kupanda na kushuka na kwa msimu huu kutokana na uzalishaji mkubwa wa ufuta nchini China ambao ni watumiaji wakubwa wa zao hilo, kumesababisha kushuka kwa bei kwa wazalishaji kutoka nchi nyingine kwakuwa uhitaji ni mdogo nchini humo.
Aidha amewasisitiza wakulima kuelekea msimu mpya wa korosho, kuhakikisha wanafuata ushauri wa wataalam kuhusu matumizi sahihi ya viautilifu.
Sambamba na hayo, Alhaji Mfaume amewasisitiza wakulima kutoa taarifa sahihi wakati wa kujisajili kwenye njia mbalimbali za malipo ili kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa malipo baada ya kuuza mazao yao, ambapo amesema kwa msimu huu changamoto hizo kwa chama cha MAMCU zimepungua kwa kiasi kikubwa na wakulima wa ufuta wameanza kulipwa fedha zao kwa wakati.