Radio Fadhila
Radio Fadhila
23 June 2025, 4:09 PM

“Kutokana na ongezeko la wateja wanaohitaji huduma ya maji kupitia MANAWASA, kumesababisha chanzo chetu kuzidiwa hivyo kulazimika kuwa na mgao wa maji ili kila mteja asikose kabisa maji“
Na Neema Nandonde
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA) inayohudumia wilaya za Masasi, Nachingwea, Nanyumbu na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Ruangwa imeeleza kuwa, inaendelea kuibua na kutafiti vyanzo mbalimbali vya maji na kuvifanyia kazi, ikiwemo chanzo cha mto Ruvuma, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaohudumiwa na mamlaka hiyo wanapata huduma ya maji kila wakati.
Hayo yameelezwa Juni 23, 2025 na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji MANAWASA Mhandisi Aneth Mawenya, alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila, ambapo amesema kuanzishwa kwa vyanzo hivyo pindi vitakapokamilika kulingana na bajeti ya serikali kutasaidia kuondoa mgao wa maji katika maeneo wanayoyahudumia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja MANAWASA Obadia Mtuya, amekiri kuwepo kwa changamoto ya kucheleshwa kwa maunganisho ya maji kwa wateja wapya kwa miezi michache iliyopita, huku kieleza kuwa sababu kubwa ilikuwa ni uchache wa mita, lakini hivi sasa vifaa vimeshafika na wateja wataunganishiwa huduma ya maji kwa wakati.
Aidha Mtuya amewataka wateja kulipa ankara za maji kwa wakati, ili kuondoa usumbufu wa kukumbushwa mara kwa mara na kuiwezesha mamlaka hiyo kuendesha shughuli zake ambazo zitarahisisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Masasi -Nachingwea (MANAWASA), toka kuanzishwa kwakwe imekuwa na ongezeko kubwa la wateja ambapo mwaka 2013 ilikuwa na wateja 3000, na mwaka 2025 wateja wameongezeka hadi kufikia 17,000, jambo linalosabisha chanzo kimoja cha maji kushindwa kutosheleza hivyo kusababisha mgao wa maji kwa wateja.