Radio Fadhila
Radio Fadhila
19 June 2025, 9:37 AM

“Familia nyingi zinaamua kukaa kimya pindi mwanafamilia anapomfanyia ukatili mtoto aliyeko ndani ya familia hiyo, kwa kuhofia kuwa wakiripoti tukio hilo mwanafamilia huyo atachukuliwa hatua“
Na Neema Nandonde
Jamii wilayani Masasi mkoani Mtwara imetakiwa kuacha kuficha matukio ya ukatili dhidi ya watoto, ili kukomesha matukio hayo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kuhusu siku ya mtoto wa Afrika juni 16, 2025 yaliyofanyika katika kipindi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Lisekese Zainabu Mtoro, ameeleza kuwa baadhi ya familia zinaficha matukio ya ukatili wanayofanyiwa watoto kwakuwa yamefanywa na wanafamilia.
Amesema kuwa, uwepo wa usiri huo unasababisha kutopatikana ushahidi wa kutosha kwa baadhi ya kesi zinazohusisha ukatili kwa watoto, jambo linaloifanya jamii iendelee kufanya matukio hayo kwa kuamini kuwa watayamaliza wenyewe kwa wenyewe, pasi na sheria kuchukua mkondo wake.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mwanzo Lisekese Lightness Masimba, ameitaka jamii kuachana na mila potofu zinazosababisha kuleta ubaguzi kwa baadhi ya watoto, jambo linalosababisha watoto kunyimwa haki zao za msingi.

Ikumbukwe kuwa siku ya mtoto wa Afrika, ilitokana na mauaji ya halaiki dhidi ya watoto yaliyofanyika nchini Afrika kusini katika eneo la mji wa Soweto Juni 16 1976, ambapo watoto wengi waliuwawa wakati wa kudai haki zao ikiwemo elimu kutoka kwa makabulu.