Radio Fadhila
Radio Fadhila
5 June 2025, 7:28 PM

Taka zinazozalishwa majumbani na viwandani, bado ni fursa kwa jamii, badala ya kuzitupa mtaani wanaweza kutengeneza mkaa mbadala ambao ni mzuri kwa afya ya binaadam na mazingira.
Na Neema Nandonde
Kutokana na kuanzishwa kwa kituo cha elimu ya mazingira kilichopo wilayani Masasi mkoani Mtwara, jamii wilayani humo inapata nafasi kubwa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu utunzaji wa mazingira na fursa zake ikiwemo kuzigeuza taka ngumu kuwa na thamani zaidi.
Akizungumza na redio Fadhila Juni 5, 2025 kuhusu siku ya mazingira duniani, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Masasi Julius Mwikaragate amesema kuwa, kupitia kituo hicho cha elimu ya mazingira kinasaidia jamii kugeuza taka ngumu na kutengeneza vitu mbalimbali ikiwemo nishati safi ya kupikia (mkaa mbadala).
Aidha ameeleza kuwa, kupitia kituo hicho cha elimu ya mazingira wataalam wanatoa elimu ya umeme jua, uhifadhi wa misitu, uvunaji wa maji ya mvua na mbinu mbali za uhifadhi wa mazingira bila malipo yoyote ili kuisaidia jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na kuona fursa zinazopatikana kupitia maliasili mbalimbali zilizopo kwenye mazingira wanayoishi.

Akizungumzia kuhusu msisitizo uliowekwa kwenye kaulimbiu ya siku ya mazingira duniani kwa mwaka 2025 inayosema “Mazingira yetu na Tanzania ijayo; Tuwajibike sasa, dhibiti matumizi ya plastiki”, Mwikaragate ameeleza athari zinazopatikana kutokana na taka za plastiki huku akiitaka jamii kudhibiti taka hizo.
Kituo cha Elimu ya mazingira kwa vitendo kilichopo wilayani Masasi mkoani Mtwara, kimeanzishwa kwa lengo la kuiwezesha jamii kufahamu athari za uharibifu wa mazingira, na namna ya kuhifadhi mazingira ili kuzifikia fursa zilizopo kwenye maeneo yao, kupitia uwezeshwaji wa miradi mbalimbali unaotolewa na kituo hicho kwa wananchi.
