Radio Fadhila
Radio Fadhila
1 June 2025, 4:54 PM

“Tatizo watanzania wengi wanatumia mazoea kwenye shughuli za kilimo, hili tumekutana nalo kwenye maeneo mengi nchini, wanavuna mahindi wanatupa chini (ardhini) kama njia ya kukausha, hii inasababisha uzalishaji fangasi wanaosababisha Sumukuvu”
Na Neema Nandonde
Jamii wilayani Masasi mkoani Mtwara imeshauriwa kuzingatia kanuni bora za kilimo na namna nzuri ya kuhifadhi chakula ili kuepuka fangasi zinazosababisha sumu kuvu, ambayo ina athari kubwa kwa afya ya binaadam ikiwemo kwenye mfumo wa uzazi.
Hayo yameelezwa Mei 27, 2025 na Afisa Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo makao makuu Dodoma, Benny Rushunju alipokuwa akizungumza na redio Fadhila baada ya kuhitimisha mafunzo ya siku 2, yaliyolenga kutoa elimu kuhusu Sumukuvu na uhifadhi wa chakula, kwa mabalozi na viongozi wa kijamii takribani 600 kutoka wilayani Masasi yaliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Masasi.
Rushunju amesema kuwa miongoni mwa athari za Sumu kuvu ni pamoja kansa ya koo, udumavu, na upungufu wa nguvu za kiume, huku akionya kuhusu matumizi ya vyakula vibichi vinavyochanganywa kwenye mfuko mmoja ikiwemo karanga, korosho, mihogo na nazi, mchanganyo unaojulikana kwa jina maarufu Powerbank, kuwa vinaweza kusababisha kuenea kwa Sumu kuvu kutoka kwenye chakula kimoja kwenda kwenye vyakula vingine.
Kwa upande wake mgeni rasmi, ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo kwa jimbo la Ndanda, Mbunge wa jimbo hilo Cecil Mwambe amewataka mabalozi waliopata elimu hiyo kwenda kuisambaza kwa wananchi, ili kuhakikisha kuwa wanafahamu namna bora ya kuhifadhi chakula na umuhimu wa kufuata kanuni bora za kilimo.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi waliohudhuria mafunzo hayo, Diwani wa Kata ya Mwena Nestory Chilumba amemshukuru Mbunge Mwambe kwa kuwezesha kupatikana kwa mafunzo hayo ambayo yatasaidia kulinda afya za wananchi wilayani Masasi.
Sumu kuvu ni kemikali sumu zinazozalishwa na fangasi wanaoingia kwenye mazao mbalimbali ikiwemo mahindi na karanga wakati yakiwa shambani au kwenye ghala.