Radio Fadhila

DC Kassanda asisitiza mabasi kuwa na madereva wawili safarini

10 May 2025, 9:20 AM

Mkuu wa wilaya ya Masasi Bi. Rachel Kassanda akiwajulia hali majeruhi katika hospitali ya wilaya Mkomaindo. Picha na Halmashauri ya Mji Masasi

Jeshi la Polisi fanya ukaguzi wa mara kwa mara wa kuhakikisha madereva wote wawili wanakuwepo kwenye mabasi yanayosafiri hasa nyakati za usiku ili kuleta ufanisi wa safari na usalama wa abiria.

Na Neema Nandonde

Mkuu wa wilaya  ya  Masasi mkoani Mtwara, Bi Rachel Kassanda ametoa rai kwa wamiliki wa mabasi ya abiria kuhakikisha wanakuwa na madereva wawili  wakati wa safari hususani nyakati za usiku ili kuepusha ajali zinazotokana na uchovu wa madereva.

Ameyasema  hayo Mei 8, 2025 alipokwenda kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya Basi la abiria kampuni ya Maning Nice lenye namba za usajili T 848 ELA iliyotokea alfajiri ya  Mei 7, 2025 katika eneo la Sululu Wilaya ya Masasi.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa kuhakikisha madereva wote wawili wanakuwepo kwenye mabasi yanayosafiri  hasa nyakati za usiku ili kuleta ufanisi wa safari na usalama wa abiria.

Akizungumza mara baada ya kuwaona majeruhi amesema kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi, ajali hiyo imetokea alfajiri ya kuamkia Mei 7, 2025 ambapo basi hilo lilikuwa linatokea Dar es Salaam kuelekea Tunduru  likiwa na dereva  mmoja  tu Elisha John (29), ambaye alikua anaendesha usiku kucha kabla ya ajali hiyo kutokea.

Aidha katika ajali hiyo,  hakuna kifo kilichotokea na kuna majeruhi 23 ambao wapo Hospitali ya Mkomaindo, na baadhi yao wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Ndanda.

Basi la abiria la Kampuni ya Maning Nice ikiwa katika eneo la Sululu ambako ajali imetokea. Picha na Halamashauri ya mji Masasi

Mkuu wa wilaya Kassanda amewapongeza madaktari kwa hatua ambazo wamezichukua katika kuhakikisha  kuwa  majeruhi wote wanapatiwa  matibabu kwa  wakati.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Masasi Dkt. Salum Gembe amesema hakuna kifo kilichotokea katika ajali hiyo na majeruhi wote wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Mkomaindo.