Radio Fadhila
Radio Fadhila
11 April 2025, 2:06 PM

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche akizungumza kwenye kipindi cha Asubuhi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila. Picha na Godbless Lucius
Hata chama cha CHADEMA kikifanikiwa kushika dola, kisipotendenda haki kwa watanzania sisi kama wanachama tutakemea na kuhitaji mabadiliko
Na Neema Nandonde
Makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa John Heche, amesema kuwa chama hicho kinafuata misingi ya katiba hivyo kuundwa kwa kundi la wanaojiita G55 wao hawahusiki nalo, na bado wataendelea kusisitiza msimamo uliotolewa na mkutano mkuu wa CHADEMA kuhusu kampeni ya No Reforms No Election.
Ameyasema hayo April 8, 2025 alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha asubuhi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila, ambapo amesisitiza kuwa msingi wa kampeni ya no reforms no Election ni pamoja na kudai mabadiliko ya tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC), kwa kile alichokieleza kuwa mabadiliko hayo yatapelekea uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Aidha amesema kuwa hata chama cha CHADEMA kikifanikiwa kushika dola, kisipotendenda haki kwa watanzania, wao kama wanachama watakemea na kuhitaji mabadiliko.
Sambamba na hayo, Heche amewatoa wito kwa wananchi kuhamasika kujaza fomu zinazolenga kupinga uchaguzi (petition form) endapo hakutakuwa na mabadiliko wanayoyahitaji, fomu ambazo zitapelekwa kwa wananchi na zikisainiwa na wananchi million 15, zitapelekwa serikalini na kwenye vyombo vingine husika ndani na nje ya nchi, ili kuwasilisha maoni hayo ya wananchi juu ya madai ya kutofanyika kwa uchaguzi mkuu kwakuwa hakuna mabadiliko kwenye INEC.